04/11/2009 8.54.53


Ulimwengu wa utandawazi ni changamoto ya Uinjilishaji mpya unaohitaji mikakati mipya ya kichungaji


|

Askofu mkuu Agostino Marchetto, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Shughuli za kichungaji kwa ajili ya wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum anasema, Kongamano la sita la kimataifa kwa ajili ya wahamiaji na wakimbizi linalenga kupembua kwa kina changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu wa utandawazi, miaka mitano baada ya kuchapisha hati ya kichungaji kuhusu wakimbizi na wahamiaji.
Kongamano hili litakuwa ni fursa kwa viongozi wa Kanisa, wanasiasa na mashirika ya kimataifa yanayotoa huduma zao kwa wakimbizi na wahamiaji kushirikishana mang'amuzi na changamoto zinazojitokeza katika ulimwengu wa utandawazi, ili kutoa jibu muafaka kwa changamoto hizi mintarafu tunu msingi za maisha ya Kiinjili.
Askofu mkuu Marchetto akizungumza na waandishi wa habari, siku ya jumanne, tarehe 3 Oktoba, 2009, wakati Baraza la Kipapa lilipokuwa linafafanua juu ya ratiba ya matukio makuu kuhusu Kongamano la sita la Kimataifa kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji. Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita aliwahi kusema kwamba, ulimwengu wa utandawazi ni changamoto kubwa katika Uinjilishaji mpya pamoja na mikakati mipya ya shughuli za kichungaji.
|