04/11/2009 9.14.03


Viongozi wa Kanisa, Mashirika ya Kimataifa, Wanasiasa na Wanadiplomasia ni kati ya washiriki wakuu wa Kongamano la sita kwa ajili ya wahamiaji na wakimbizi


|

Monsinyo Novatus Rugambwa, Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa ajili ya wahamiaji, wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi maalum, akizungumza na waandishi wa habari siku ya jumanne, tarehe 3 Novemba, 2009 kuhusu Kongamano la sita la kimataifa kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji anasema, hii itakuwa ni fursa ya kuweza kusikiliza mang'amuzi na changamoto kutoka kwa wazungumzaji kumi na nne walioalikwa rasmi na Baraza lao.
Kongamano hili linahudhuriwa na Maaskofu hamsini na tatu wanaohusika kwa karibu zaidi na huduma kwa wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi. Mapadre hamsini na saba, watawa kumi na sita na walei kumi na tisa watarajiwa kushiriki. Jumla ya wawakilishi kutoka Mabaraza ya Maaskofu Katoliki watakuwa ni mia moja na arobaini na nne. Mashirika ya kitawa yatawakilishwa kikamilifu kwani hawa wamekuwa mstari wa mbele katika utoaji wa huduma kwa wahamiaji, wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi maalum.
Monsinyo Novatus Rugambwa anaendelea kubaini kwamba, Kongamano la sita la kimataifa, litayashirikisha pia mashirika ya kimataifa kutoka Umoja wa Mataifa, Mashirika ya Kimataifa ya Huduma kutoka Kanisa Katoliki pamoja na wataalam, kwa pamoja watashirikiana bega kwa bega na Baraza hili la Kipapa, ili kufanikisha Kongamano hili.
Mabalozi kadhaa wanaowakilisha nchi zao mjini Vatican wanatarajiwa pia kuhudhuria. Kimsingi anasema Monsinyo Rugambwa ni kwamba, kutakuwa na watu mia tatu na ishirini wanaotarajiwa kuhudhuria Kongamano la sita la kimataifa kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji katika ulimwengu wa utandawazi.
|