HomeRadio Vaticana
foto testata  

Categories


  Charity & Solidarity


  Church


  Culture & Society


  Vatican Documents


  Synod


  Ecumenism


  Family


  Youth


  Justice & Peace


  Politics


  Religion & Dialogue


  Science & Ethics


  Audiences
   & Angelus



  Pastoral visits


cx_t06

CTV - You tube

CTV



 home > Church > news


05/11/2009 12.09.52



Benedikto XVI anawaalika waamini kuyaelekeza macho yao nyumbani kwa Baba kwa imani na matumaini






Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita siku ya alhamisi, tarehe 5 Novemba, 2009 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea marehemu makardinali, maaskofu wakuu na maaskofu waliofariki dunia katika kipindi kuanzia Mwezi Novemba, 2008 hadi kufikia Novemba, 2009, akiwaasa waamini kuyaelekeza macho yao nyumbani kwa Baba wa mbinguni, ulikokusanyika umati mkubwa wa watakatifu.

Katika mahubiri yake Baba Mtakatifu anasema, Siku kuu ya Watakatifu wote inayofuatiwa na Siku ya kuwaombea waamini wote marehemu ni siku ambazo waamini wengi wanaziishi kwa kukazia zaidi imani inayomwilishwa katika maisha ya sala, ili kufahamu Fumbo la Maisha ya Kanisa kwa ujumla na changamoto ya kuwa macho, mwanadamu anapoendelea na hija ya maisha yake hapa duniani kuuendea uzima wa milele.

Baba Mtakatifu amewataka Makardinali ambao tayari wamekamilisha hija ya maisha yao hapa duniani kuwa ni Kardinali Avery Dulles, Pio Laghi, Stephanos II Ghattas, Stephen Kim Sou-Hwan, Paul Joseph Pham Dinh Tung; Umberto Betti, Jean Margèot pamoja na umati mkubwa wa maaskofu wakuu na maaskofu walioitupa mkono dunia katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Baba Mtakatifu anasema, Kanisa linawatolea Sadaka ya Ekaristi Takatifu kama kawaida ya kila mwaka, kwa kukumbuka zaidi umoja unaoonekana na ule unaofumbatwa katika fumbo la imani, linalowaunganisha waamini walioko bado safarini hapa duniani na wale ambao tayari wametangulia mbele ya haki, kwani kifo hakiwezi kuvunjilia mbali kifungo cha udugu wa kiroho unaopata chimbuko lake katika Sakramenti ya Ubatizo na Daraja Takatifu.

Baba Mtakatifu anasema viongozi hawa wa Kanisa wanakumbukwa kutokana na utume wao, watu ambao wameyamimina maisha yao kwa ajili ya Kanisa, wakihakikisha kwamba, waamini wanapata mahitaji yao msingi; mashahidi wa Injili kwa kushirikisha karama na tunu za maisha yao wakati wa kutekeleza majukumu yao ya kichungaji, kwanza kabisa kama Waamini, baadaye kama Mapadre, hao ndio wanaoshirikishwa sasa Karamu ya Uzima wa milele, ambayo kwayo Yesu Kristo anajitoa mwenyewe kuwa ni chakula; anafutilia mbali mauti na kuwakirimia waamini maisha yake yasiyokuwa na mwisho, changamoto ya kuendelea kukesha, ili atakapokuja Bwana awakute wangali macho.

Baba Mtakatifu anasema roho zao wenye haki wamo mikononi mwa Mungu, wala maumivu hayatawagusa, wako katika amani na matumaini ya uzima wa milele, kama imani ya Kanisa inavyofundisha. Maisha ya mwanadamu yanasheheni matatizo, mahangaiko, machungu na nyakati ngumu ambazo, mwamini anaalikwa kuzipokea na kuzikubali, kama sehemu ya maandalizi ya maisha ya uzima wa milele. Waamini wanakumbushwa kwamba, hapa duniani wao ni wasafiri na kamwe hawana makazi ya kudumu.

Katika hija ya maisha yao hapa duniani, Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuwa na matumaini hai ambayo kamwe hayadanganyi. Mtakatifu Petro katika waraka wake wa kwanza kwa watu wote anawaalika waamini kufurahi katika Mungu Mwenyezi, Baba wa Yesu Kristo ambaye amewazaa mara ya pili ili kupata tumaini lenye uzima kwa kufufuka kwake Yesu Kristo kutoka katika wafu; wapate urithi usiharibika, usiokuwa na uchafu, usionyauka na uliotunzwa mbinguni kwa ajili yao.

Baba Mtakatifu anasema hiki ndicho kiini cha furaha kwa waamini, hata kama wanakumbana na shida na magumu mbali mbali ya maisha. Changamoto ni kuendelea kudumu katika imani, iliyosafishwa kwa majaribu mbali mbali, lakini siku moja itang'ara na kutoa kishindo cha masifu na utukufu, Kristo atakapokuja katika utukufu wake.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita alizikabidhi roho za waamini Makardinali, Maaskofu wakuu na Maaskofu, waliotekeleza utume wao ndani ya Kanisa kwa huruma ya Mungu. Wasamehewe mapungufu yao ya kibinadamu na hatimaye, waweze kupokelewa mbinguni kwenye uzima wa milele, ili wapewe tuzo la haki.

Bikira Maria awasindikize kwenye mlango wa Paradiso na aendelee kuwasaidia waamini wengine ambao bado wako safarini kuwa macho, viuno vyao vikiwa vimefungwa, taa zao zikiwaka, tayari kumlaki Bwana atakapokuja wakati wowote ule.


  « back to index

 






05/11/2009 18.17.53
Pope Prays for Departed Cardinals and Bishops


05/11/2009 15.49.19
The General Prayer Intention of the Church for November is that all may be part of the commitment to safeguard Creation.


04/11/2009 15.36.45
Debate is necessary but the Truth must prevail, said Pope Benedict at the midweek General Audience.


04/11/2009 11.03.01
Benedikto XVI kuongoza Ibada ya kuwaombea marehemu Makardinali na Maaskofu Siku ya Alhamisi asubuhi


04/11/2009 10.11.37
Taarifa ya ziara ya mkaguzi wa kitume kwa mashirika ya kitawa nchini Marekani: matumaini na wasi wasi kwa siku za usoni!



Related categories


Page précédente  Previous page
Page d'accueil  Home Page
Ecrire à la rédaction  Contact us
top
top
All the contents on this site are copyrighted ©. Webmaster / Credits / Legal Conditions
top
top