07/11/2009 9.44.36


Michezo ni sehemu ya utangazaji wa Habari Njema na Majiundo ya kimaadili na kiutu


|

Kardinali Stanslaw Rylko, Rais wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya walei anasema, imani inaweza kuleta mwelekeo mpya katika katika shughuli za michezo na utamaduni. Michezo kwa miaka mingi imekuwa ni sehemu muhimu kwa ajili ya majiundo ya vijana duniani, jambo ambalo linaungwa mkono pia na Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kama njia ya kuboresha tunu msingi za maisha adili na kiutu.
Idara ya michezo ya Baraza la Kipapa kwa ajili ya walei, limeandaa semina maalum inayoongozwa na mada: michezo, elimu na imani, mwelekeo mpya katika shughuli za michezo ndani ya Kanisa Katoliki. Lengo la semina hii ni kuwawezesha wahusika kutambua uhusiano uliopo kati ya michezo, majiundo ya binadamu na imani mintarafu vyama vya michezo vinavyosimamiwa na kuongozwa na Kanisa Katoliki.
Kardinali Ryliko anasema, hata katika michezo Kanisa bado linaendelea kutoa mchango wake wa dhati kama sehemu ya Uinjilishaji na majiundo endelevu ya mwanadamu. Hii ni mara ya tatu kwa Baraza la Kipapa kwa ajili ya walei kuandaa semina inayohusu Kanisa na michezo.
Michezo inapaswa kupewa umuhimu wake ndani ya Kanisa na kamwe isionekane kuwa ni sekta inayotishia maisha na utume wa Kanisa, lakini michezo ina mvuto wa pekee kwa vijana hata katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa. Baadhi ya wazazi wanachukulia fursa ya michezo kama sehemu ya burudani kwa vijana hasa baada ya pilika pilika za maisha ya shule na kazi.
Lakini wengine wana maono tofauti kwani, kwa wazazi wenye watoto wenye vipaji katika michezo ni nafasi kwa watoto hao kupata umaarufu kwa siku za usoni, hali inayokwenda sambamba na ubora wa maisha. Kardinali Rylko anasema, Mama Kanisa anapaswa kuendelea kutoa msukumo wa pekee katika shughuli za michezo kama njia ya utangazaji wa Habari Njema na majiundo ya mwanadamu. Imani ikimwilishwa katika michezo inaleta utofauti katika matukio haya.
|