07/11/2009 10.54.39


Imani thabiti ilichangia kuanguka kwa ukuta wa Berlini, miaka ishirini iliyopita!


|

Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican anabainisha kwamba, imekwisha yoyoma miaka ishirini tangu ukuta wa Berlini uliopobomolewa na hivyo kubomoa pia vikwazo dhidi ya uhuru wa mwanadamu, jambo ambalo lilipelekea maelfu ya watu kupoteza maisha yao wakijaribu kuvuka ukuta wa Berlini.
Watu wengi walidhani kwamba, gereza hili lililokuwa linalindwa kwa mlango wa chuma lingeweza kudumu kwa miaka kadhaa, lakini wapi! Hii inatokana na ukweli kwamba, watu walikuwa na uhuru tenge uliojengeka katika falsafa dhidi ya uwepo wa Mungu na mwanadamu katika maisha ya watu wa Ulaya ya Mashariki. Ukuta wa Berlini ulianguka na kwa bahati nzuri, kulikuwa hakuna umwagaji mkubwa wa damu ya watu wasiokuwa na hatia.
Bila kutegemea, Jumuiya ya Kimataifa ikaanza mchakato mpya wa historia, hali inayokumbusha dhamana na uwepo wa Hayati Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa pili, hija zake za kichungaji nchini Poland, mahali ambapo watu waliendelea kuwa wajasiri katika imani yao kwa Kanisa Katoliki na jitihada za kutafuta uhuru wa kweli kwa majirani zao.
Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa pili aliikumbusha Jumuiya ya Kimataifa kwamba, Kanisa kwa njia ya imani yake iliiwezesha Ulaya ya Mashariki na Magharibi kuungana tena, mchango wa Kanisa kwa Bara la Ulaya dhidi ya Ukanimungu. Kwa hakika, imani haiwezi kubinafishwa na kuwekwa kibindoni.
Kwa bahati mbaya anasema, Padre Federico Lombardi kwamba, kuna watu duniani walijenga na wanaendelea kujenga kuta za utengano. Lakini, Kanisa litaendelea kwa matumaini kusubiri kusherehekea kuporomoka kwa kuta ambazo hazina mafao katika maisha ya mwanadamu.
|